Sunday, September 4, 2016

Ahadi za Rais Magufuli Zenji

Tags

MO Blog imekuandika mambo aliyoyaahidi Rais John Pombe Magufuli wakati akihutubia wananchi katika viwanja vya Kibanda Maiti kisiwani Unguja ni pamoja na kuifanya Zanzibar kuwa makao makuu ya viwanda vya samaki na hoteli za kitalii.
Dk. Magufuli amesema ameshaanza kutafuta wawekezaji, na kwamba amekwisha zungumza na baadhi ya wawekezaji ambao wamemkubalia kujenga viwanda vya samaki na hoteli kubwa na za kisasa za utalii.
Rais Magufuli amesema kuwa “Zanzibar imezungukwa na maji, viwanda vingi vikijengwa itasaidia kuinua wavuvi, pia hoteli zikijengwa watalii watakuja, vijana wote watapata ajira bila kujali itikadi zao, pia uchumi utakua. “
Ahadi nyingine alizozitoa ni kuharakisha upitishwaji wa sheria za mafuta na gesi ili zifanye kazi.
“Nimezungumza na wahusika kuhusu kuharakisha upitishwaji wa sheria za gesi, nataka mafuta na gesi yachotwe hapa ili Zanzibar itajirike, nahangaika kutafuta wawekezaji na nashukuru wananielewa,” amesema.
Kuhusu tatizo la uhaba wa maji visiwani humo, Magufuli amesema amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Libya ambaye ameahidi kutoa zaidi ya bilioni 200 kwa ajili ya kuanzisha mradi wa maji visiwani humo.
Dk. Magufuli amesema kuwa, mradi huo utaanza siku za hivi karibuni kwa kuwa pande zote mbili zimekwisha saini mkataba.
Hata hivyo, Rais Magufuli alisema mradi wa maji unaofadhiliwa na benki ya Afrika unaogharimu dola za kimarekani milioni 21, umeshaanza kutekelezwa na kwamba vitajengwa visima 11 huku 21 kukarabatiwa pamoja na kujenga miundombinu ya mabomba yenye urefu wa kilomita 153.
Kwa upande wa miundombinu ya barabara, amesema serikali kuu kwa kushirikiana na serikali ya visiwani Zanzibar, itatoa bilioni 10 kwa ajili ya kukarabati barabara zilizoharibika.
Vile vile amesema atatoa ushirikiano kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Alli Mohammed Shein ili kuharakisha maendeleo ya visiwa hivyo.
Dk. Magufuli amewashukuru wakazi wa Unguja kwa mapokezi mazuri huku akitoa wito kwa viongozi wa dini kuwaombea wanaokwamisha jitihada za serikali za kuleta maendeleo.
“Nasema nawashukuru kwa mapokezi makubwa, nawashukuru wote, nipo pamoja na nyinyi kulisukuma gurudumu la maendeleo yetu,
“Wito wangu tushikamane, tuwe wamoja katika maendeleo, unapozungumzia maendeleo wakati watu hawana maelewano hayawezi yakaja,” alisema na kuongeza.
“Niwaombe viongozi wa dini muwahubirie hawa watu wanaotuchelesha kwenda mbele, muwaombee dua watu wanaokwamisha maendeleo.”


EmoticonEmoticon